Nenda kwa yaliyomo

Mwaka wa Kanisa

Kutoka Wikipedia, kamusi elezo huru
Pitio kulingana na tarehe 11:35, 15 Aprili 2012 na Kipala (majadiliano | michango)
Mwaka wa Kanisa kadiri ya kalenda ya liturujia ya Roma

Mwaka wa Kanisa (pia: mwaka wa liturgia / liturujia) ni mpangilio wa muda au kalenda inayoratibu sikukuu za kikristo katika muda wa mwaka 1.

Kalenda hii inataja nafasi ya vipindi kama vile majilio (adventi) au kwaresima, na pia nafasi ya sikukuu. Sikukuu kadhaa kama Krismasi zinafuata tarehe za kudumu za kalenda ya jua lakini nyingine kama Pasaka ni tarehe zinazozogezwa katika kalenda ya kawaida hasa kwa sababu zinafuata hesabu ya Jumapili si tarehe katika mwezi fulani.

Mwaka wa kanisa na madhehebu

Si makanisa yote ambayo yanaangalia hesabu ya mwaka wa kanisa kwa jumla lakini karibu zote zinasheherekea sikukuu kubwa kama Krismasi, Ijumaa Kuu na Pasaka kufuatana na utaratibu wake. Kimsingi kuna mahesabu mbili:

  1. mapokeo ya magharibi kwa kanisa katoliki na Waprotestanti kama Anglikana, Walutheri, Wapresbiteri, Wamoravian;
  2. mapokeo ya mashariki kwa makanisa ya Kiorthodoksi
  3. makanisa kadhaa ya kale ya mashariki huwa na sikukuu na vipindi maalumu mfano Wakopti au Kanisa la Uhabeshi.

Tofauti kati ya mapokeo ya magharibi na masharioki kimsingi ni matengenezo ya kalenda ya Juliasi kuwa kalenda ya Gregori; kanisa katoliki na Waprotestanti wamepokea kalenda ya Gregori lakini Waorthodoksi wanaendelea kutumia kalenda ya Juliasi iliyotangulia.

Muundo wa mwaka wa kanisa

Muundo wa kalenda hii ya mwaka wa kanisa unasimama juu ya sikukuu kubwa mbili za Krismasi na Pasaka na vipindi vya siku vinavyofuatana nazo.

Hesabu hii inaanza na jumapili ya kwanza ya majilio (adventi) katika mapokeo ya magharibi ambayo ni hesabu ya kwawaida kwa wakristo wengi wa Afrika ya Mashariki. Mwisho wa mwaka wa kanisa ni Jumapili kabla ya majilio inayosheherekewa kama sikukuu ya kutazama milele au kurudi kwake Kristo katika madhehebu mbalimbali.

Krismasi na kipindi chake inategemea tarehe yake ya 25 Disemba (magharibi) au 6 Januari (mashariki). Jumapili ya nne kabla ya Krismasi ni majilio ya kwanza yaani chanzo cha kipindi cha kujitayarisha kwa sikukuu hiyo. Mwisho wa kipindi cha Krismasi ni moja ya jumapili baada ya Epifania.

Kipindi cha Pasaka kinabadilika tarehe kila mwaka kwa sababu Pasaka yenyewe inategemea hesabu ya Jumapili pamoja na kutazama jua na mwezi yaani aina mbili tofauti za kalenda: ni jumapili ya kwanza baada ya mwezi mpevu wa kwanza unaotokea baada ya sikusare ya 21 Machi. Ijumaa Kuu ina kumbukumbu ya kifo cha Yesu ni Ijumaa kabla ya Pasaka.

Siku 40 kabla ya Pasaka ni kipindi cha Kwaresima kwa ajili ya maandalizi ya kumbukumbu hiyo ya kusulibiwa na kufufuka kwake. Lakini hesabu ya siku 40 inaacha jumapili katika kipindi hiki. Kwaresima inaanza kwenye Jumatano kabla ya jumapili ya sita kabla ya Pasaka.

Kipindi cha Pasaka kinakwisha kwenye jumapili ya Pentekoste[1]; pentekoste (maana ya neno ni "50" inatokea takriban siku 50 baada ya jumapili ya Pasaka.

Vipindi vingine kati ya vipindi vya Krismasi na Pasaka ni majira bila tabia maalumu, lakini hapa kuna sikukuu ya kimadhehebu zinazoweza kutofautiana kati ya kanisa na kanisa.

Maana ya mwaka wa kanisa

Ufuatano wa sikukuu unatunza kumbukumbu ya tarehe muhimu katika maisha ya Yesu jinsi zinavyosimuliwa katika Biblia.

Wakati dunia inapozunguka kandokando ya jua hadi kurudi ilipokuwa, jumuia ya wafuasi wa Yesu inazunguka kandokando yake ili kuzidi kumfahamu kwa imani, kumuadhimisha kwa tumaini na kumfuata kwa upendo.

Marejeo

  1. makanisa mengine yanaendelea hesabu yake hadi jumapili ya utatau ambayo ni jumapili baada ya Pentekoste

Viungo vya nje